Mgeni huyo alifika na kubisha hodi akiwa anamtafuta Gotta Irie. Akiwa na macho ya kujiamini huku maongezi yake yamejaa maneno yaliyokuwa na mpangilio na uhakika
Nilimkaribisha na kujitambulisha pia nilimuomba tukae 'Ze Corner' (ambayo ni sehemu ya The Irie Entertainment Center).
Swali lake la kwanza lilikuwa 'Ndio wewe Gotta Irie uliyekuwa unatangaza kipindi cha RoadBlock?' Akilini mwangu nilisema 'Haya tena, ndio wale wale ambao wanaulizia lini nitarudi kutangaza kwenye redio na blah, blah nyingi kuhusu wakati ule.'
Akaniambia 'Sauti ni ile ile, lakini siamini maana sijawahi kukuona.'
Bila kutambua ni mtu gani nimekaa nae, niliamua kujenga urafiki kwa kuhakikisha anapata urahisi wa mazungumzo. Aliniuliza mambo mengi ambayo yalikuwa ya miaka ya 1998 hadi 2002; muziki wa wakati huo, aliuliza kuhusu Umoja Family n.k.
Akauliza tena kama mimi ni Gotta Irie.
Alipopata uhakika, alifunguka na kujitambulisha. Lakini alitamka maneno yenye uzito fulani. Aliniambia kuwa '... naamini kuwa hakuna binadamu yeyote duniani anayeweza kuamini 'ukweli' wangu, ndio maana nimekutafuta mpaka nimekupata.' Nilimsikiliza kwa makini. 'Kaka nimetumika, lakini roho yangu ni safi kabisa. Sikuwa na kosa lakini nimekaa jela kwa uonevu mkubwa. Kaka, Nimesamehe.'
Alinieleza mazingira aliyokutana nayo, na alivyosingiziwa kuwa ni jambazi na kufungwa kimakosa au kwa uonevu. Bila ya kupata nafasi ya kujieleza au kujitetea. Alitumikia kifungo cha miaka nane na nusu. Alipotoka tu alihakikisha ananitafuta mpaka ananipata. Ilimtumia miezi saba hadi siku hiyo tulipokutana.
Mazungumzo yalitawaliwa na maisha ya jela na RoadBlock.
'Kaka, siku ya kwanza tuliingizwa jioni. Ilipofika saa tatu usiku baadhi yetu tulikaa kimya na kusikiliza redio kwa masaa matatu bila ubishani, kelele au kusumbuliwa na askari. Ulifanya usiku ule nione kuwa matumaini yapo hata kama mimi nilikuwa mfungwa toka siku ile.'
Nilianza kutega sikio kusudi nisikose neno.
'Kaka, RoadBlock ilijenga adabu fulani kule jela. Tulipata namna ya kuhonga askari jela na wao walitupa nafasi ya kusikiliza RoadBlock.'
Alinieleza jinsi wafungwa walivyokuwa wanakaa pamoja kujadili muziki na maneno ya yaliyokuwa yanatamkwa. Maneno ya matumaini, muziki ulioleta tafakari.
'Kaka jinsi ulivyokuwa unaongea na hiyo sauti yako - ulikuwa unatufanya tujiamini maana siku hiyo ulisema "hakuna anayeweza kuiumiza nafsi yako ila wewe mwenyewe" - siwezi kusahau.'
Alichukulia RoadBlock kama kitabu kilichojaa maandiko chanya kuhusu maisha.
'Kaka haukuwa na uwoga.'
Hadithi yake ilikuwa ya muda wa saa moja na nusu ambayo ilifungua dirisha katika ubongo wangu na kuniwezesha kuona dunia ambayo nilikuwa sijawahi kuona. Alichonisimulia kilinionyesha jinsi nafasi ya RoadBlock ilivyogusa nafsi za baadhi ya wale waliokuwa wanasikiliza. Nilimuahidi nitaendelea kuwasilisha bidhaa zinazotengenezwa kwenye ubongo kupitia nafasi zilizo finyu kufikia wahitaji. Kwa kifupi ni - nitaandika ufahamu kama ilikvyokuwa kwenye RoadBlock.Ni mengi sana tulibadilishana, na nitayaweka kama sehemu ya kitabu cha RoadBlock.
Aliniambia kuwa 'show ya mwisho kuisikiliza ilikuwa ni siku ulipozungumzia kuhusu msanii aliyewahi kufungwa na kutumia muda wake jela kusoma vitabu na majarida. Alipotoka alikuwa na ufahamu na uelewa mkubwa.'
Nitaandika.
Pamoja kaka
ReplyDelete