Friday, October 11, 2013

Super Cat - Nguzo ya dancehall.


Baada ya Yellowman na Josey Wales kutawala katika miaka ya mwanzo ya 1980, niliwafuatilia wengi waliokuwapo wakati huo; na waliofuata baadae. Papa San aliibuka na kuleta speed, stamina na story, wakati huo huo Chaplin alihubiri na kuchekesha kila alipopita. Alikuwapo Peter Metro, Burro Banton, Stitchie na wengine wengi walioshikilia dancehall. Walikuwapo chanters, deejays na singers.....
Lakini walioteka sikio langu walikuwa Mkongwe Nicodemus, Doctor Early B na mkorofi Super Cat. Ninamuita mkorofi, maana asili yake inaruhusu - mchanganyiko wa Mhindi na Mwafrika; na katika dancehall deejays - hakuna aliyewahi kutokea.
Nilivyomsikiliza Early B, alikuwa mtu mwenye kichwa cha ajabu unapokuja kwenye utunzi. Kwanza alikuwa na sauti ya kipekee, na uwezo wa kupita kwenye njia za midundo bila shida kubwa. Mwanzilishi wa uimbaji wa staili tofauti tofauti. Kusimulia matukio ya jamii kufuatana na mazingira na muda ndio vilikuwa vitambulisho vikubwa vya Doctor Early B. Mfano wimbo wake wa 'Wheelie Wheelie' ambao anazungumzia wapanda baiskeli. Anaanza kwa kuwashukuru na kuwapongeza wapanda baiskeli wa mtaani, ambao walikuwa wanawashangaza na kuwaburudisha watu mtaani kutokana na jinsi walivyokuwa wanabinuka na kupinduka na baiskeli zao; pia hao wapanda baiskeli walikuwa wasumbufu kwa polisi. Amewataja wapanda baiskeli David Weller na Xavier Miranda ambao walishinda medali na mashindano mbali mbali kama Olimpiki, Madola n.k.
Alichofanya Early B, ni kuiweka historia katika muziki. Kuongelea watu na matukio ya jamii katika wimbo na kumfanya msikilizaji kuridhika na maelezo ulikuwa uwezo mkubwa wa Early B, alikuwa mchekeshaji pia. Sikiliza C-Bert, anamzungumzia mchekeshaji anayechekesha watu hadi vifungo vya suruali kupasuka. Huyu jamaa ndiye aliyekuwa mwalimu wa Super Cat.

Super Cat ana historia ndefu na muhimu katika dancehall - kuanzia kwenye sound system, maonyesho na kwenye rekodi pia. Baada ya kupotea kwa miaka kadhaa - Super Cat aliibuka ghafla kwenye show ya Shaggy huko New York na kupagawisha washabiki waliojazana ukumbini. Angalau muonekano wake umebadilika, lakini uwezo wake wa kutawala jukwaa bado upo. Hivi sasa amekubali kuwapo katika Miaka 30 ya Sting - onyesho la siku moja na kubwa sana huko Jamaica. Pia ni onyesho lenye historia ya mapambano ya wasanii - kama la mwaka 1991 alipopambana na Ninjaman, ambaye pia atakuwapo kwenye onyesho hilo mwezi wa kumi na mbili.
Ukweli ni kwamba, ninasubiri kwa hamu kubwa kuona maonyesho ya Super Cat; ambaye mara ya mwisho nilimuona akiwa katika ziara pamoja na Kriss Kross mwaka 1992.
Mengi sana yameandikwa kuhusu Super Cat 'Wild Apache' - ni ushindi kuona mkongwe anatoka katika yale aliyopitia na kurudi mbele ya washabiki wake.


No comments:

Post a Comment