Sunday, August 10, 2014

Mwanzo wa kuvuma: Na Vitali Maembe.

Vuma!


Katikati ya mwezi Julai 2014 niliwasiliana na Vitali na akaniambia baada ya siku mbili atakuja studio, anazo nyimbo anataka kurekodi. Mimi nilimeza maneno yake kupitia masikio yangu, nikaendelea na shughuli za kawaida.
Baada ya siku mbili Maembe alinipigia simu kunieleza kuwa yupo njiani anakuja studio. Hadi muda huo nilikuwa sijajitayarisha kwa ujio wake. Haikuwa tatizo. Wakati natafakari nini kitafanyika, Nelly akanipigia simu kunieleza kuwa anakuja studio. Ilikuwa afadhali sana maana wiki hiyo nilimtegemea Nuru atakuwapo studio kwa kadhaa zilizokuwapo kipindi hicho. Na mimi niliwasiliana na 'Mugabe' (aka Sindimba Tete) tuweze kupata uwepo wake pia.
Kwenye muda wa saa tano, Maembe alifika na vijana wake wawili - Hussein na mwingine yule anapiga ngoma. Nakumbuka hatua za mwanzo za 'kuvumisha' zilianza kwa ushiriki wangu kidogo baada ya hapo Nelly aliendelea.



 
Tarehe 2 Agosti 2014, Maembe aliingia kwenye ukumbi wetu hapa 'The Corner' kama mtoa burudani; alikuja na vijana wake kama kawaida - midundo ya muziki 'live' ilisikika. Kwa kuwa John Vocal na Tete wapo mtaani kwetu, waliwasindikiza wageni wetu katika kutoa burudani. Siku hiyo ilikuwa ya uzinduzi wa 'The Corner' - jamii iliburudika.
Waliendelea kurekodi studio hadi tarehe 8/8/2014 ndio nilipousikia wimbo 'Vuma'; niliskia kweli unavuma. Nilijua nitaandika kuhusu wimbo huu, na watu kadhaa walitokea kwenye akili yangu. Na walitokea akilini kwa sababu nyingi tu - ndio zilizopelekea kundelea kuandika.
Nilimkumbuka rafiki yangu Innocent Mnyuku kwa makala moja aliwahi kuandika kuhusu 'Usiku Wa Umoja' uliojumuisha wasanii na vikundi mbali mbali kama vile Zemkala, Vitali Maembe & The Spirits, Gwandumi na Machifu Band..... wengine nimesahau. Huyu jamaa mara nyingi anatoa msisitizo kwangu kuwa nisiache kuandika.
Nilimkumbuka dada 'angu Irene Sanga, maana toka wakati alipotoa album yake ya UTANDAWAZI, sijasikia wimbo uliofanana na 'Wanapangisha' kutokana na nini kimeshibishwa kwenye wimbo. Mpangilio wa vyombo, sauti, na zaidi 'kalamu' - kwa maana ya utunzi.
Niliwakumbuka Jhiko Manyika na Gwandumi ambao ninafahamu uwezo wao na misimamo yao kimuziki na majukumu yao kwa jamii. Pia ni wahitimu wa Bagamoyo College of Arts.

Hapo juu nimeandika kuwa 'nilisikia kweli unavuma' kwa maana tofauti. Kwa sauti za vyombo, nyuzi butu limevuma kwa kiwango. Ushuhuda ninao maana nilikuwapo wakati Tete analivurumisha. Utunzi ni jambo lingine linaloufanya huu wimbo uvume. Wakati muafaka - jamii ipo katika kipindi cha 'kuwekana sawa' kuhusu Muungano, Katiba n.k.
"Kumbe imekwisha, kumbe imetoweka amani. Kumbe imepita."
Hayo maneno yalirudisha kumbukumbu ya miaka ya nyuma, toka wakati wa utoto wangu hadi hivi sasa. Yalinifanya nitambue nini nilichopata. Hayo maneno yalitaka niingiwe na uwoga wa kupoteza/kuishiwa/kutoweka kwa amani. Je imekwisha? Nilijuliza!!
Nilisikiliza tena wimbo huo - nikaamua kuuweka katika makundi mawili; kundi la kwanza ni utabiri na kundi la pili ni rekodi. Rekodi inayowekwa kwa ajili ya kukumbusha hisia za jamii yetu kwa wakati uliopo.


No comments:

Post a Comment