Irie Productions
Mwaka 2009, nilianza kutengeneza studio za Irie Productions, huku kwetu Tegeta. Hii ilikuwa miaka miwili baada ya projects tulizofanya tulipokuwa na akina Tony pale ActiveAudio - Manzese. Mwaka 2011 ndio nilifungua milango kwa jamii kuweza kurekodi kazi zao, wakati huo hakuna ala - zaidi ya Akai MPK61 na iMac. Tulitoa nafasi kwa wasanii wa hapa jirani na mazingira yetu; na jaribio hilo halikuwa na matunda. Maana wengi walihitaji hatua zaidi ya kurekodi tu. Walihitahi label na promosheni za redio.
Marafiki, ndugu na jamii ya wasanii; na kwa kiasi fulani wale waliopo kwenye fani ya habari. Walikuwa wananishauri na kuniambia kuwa nina msimamo usioeleweka - kwa nini nisifanye kwa kiwango kikubwa. (Nikafikiria - 'ukubwa wa pua sio wingi wa kamasi'). Wewe Gotta unafahamika, unaweza kufanya vitu kadhaa, unajuana na watu wengi. (Nikafikiria - 'sitaki wanijue mimi, lakini nataka wajue nini kitatoka Irie Productions').
Hivi sasa tumeongeza ala, na Nelly alibuni na kutengeneza sound proof. Tumeweza kufanya kazi na wasanii/wanamuziki kadhaa. Ambayo imekuwa faraja. Lakini falsafa ya Irie Productions haijabadilika na haitobadilika kwenye hii miaka yetu, ni hapo baadae (kama miaka themanini ijayo, maana mtazamo utakuwa umekamilika na falsafa imekomaa).
Ninatoa mfano wa falsafa yetu!
Tulipoanza kurekodi 'Vuma' wimbo wa Vitali Maembe; tulianza kimya kama sehemu nyingine inavyotokea. Baada ya kumaliza kurekodi, mashine (computer) ilipata matatizo. Lakini wimbo ulikuwa tayari. Tuliusikiliza pamoja na baadhi ya wadau, na wengi walipendekeza tuupeleke kwenye redio haraka sana. Maana wimbo upo na wakati na mazingira halisi - kwa maana ya mambo yanayotokea katika taifa letu hili.
Lakini tulichofanya ni kuacha kila kitu kiendelee kama kilivyoanza. Tuliweka wimbo kwenye ukurasa wa Irie Productions (SoundCloud), na tuliuweka kwa wiki moja kwa watu kusikiliza. Baada ya hapo tuliruhusu download. Pia tuliwaomba wale ambao walitaka tuwatumie kwa e-mail wawasiliane nasi. Tulianza kuusambaza namna hiyo. (Iga ufe!)
Internet radio stations ziliukubali na kuanza kupiga, baada ya hapo ulianza kusikika kwenye redio zetu za FM. Hapo ndipo tulipokaa na uongozi wa Times FM, na kukubaliana vitu vichache. Hayo makubaliano ndio yaliyoifikisha bendera ya redio hiyo juu ya Mlima Kilimanjaro.
Hivi sasa imefika wakati wa 'lawama'. Kwa nini haujatuletea wimbo redio yetu? Ah, Gotta kwa nini unafanya hivyo?
"Kama sijafahamu jukumu lako, nitajuaje unachotaka?"
Ni falsafa nyepesi. Na hii itadumu kwa muda mrefu sana. Na hii itatufikisha mbali sana. Na hii itakufikisha mbali kuliko wengine!



No comments:
Post a Comment