Umeibuka mjadala kama sio 'kona' ya mabadiliko katika tasnia ya muziki Tanzania. Nimeita kona ya mabadiliko kwa sababu umefika wakati wa wadau kuelewa na kuelimika kwa upana kuhusu biashara ya burudani na mfumo wake katika nchi yetu hii. Wakati tunajadili sababu, matokeo na maendeleo ya tukio/matukio - lakini hakuna kitu au mtu ambaye ameonyesha ishara ya kuangalia mazingira yaliyopo kwa ajili ya kuepuka hatari ya mpasuko mkubwa zaidi. Kama tutaruhusu mpasuko mkubwa, itakuwa ni hasara kwa vizazi vinavyokuja. Kuna sheria na taratibu ambazo zinatakiwa kuzingatia kwenye biashara ya burudani kwa ujumla. Ushabiki unaotokea umefunika/kuficha ukweli kuwa yanayoendelea hayatakiwi kuwajadili wahusika, ila kurekebisha uchafu huu. Nitatoa mfano ambao tunaweza kupata picha ya haya mazingira, na kuweza kujiweka sawa kukabiliana na yatakayokuja baadae.
Tujaribu kuangalia mazingira ambayo wanausalama wamekufuata na kuanza kukushika na kukusukuma au hata kukupiga kofi. Uwe una kosa au hata hauna kosa. Lakini kwa uwoga wako, unatishika na kusalimu amri. Swali, je haki ipo wapi? Kwa yule mwanausalama kukusukuma na kukushika, au wewe kujua sababu? Unaweza kukuta pande zote mbili hazitambui haki na taratibu. Upande wa mwanausalama anona ni wajibu wake kukukamata kwa namna yeyote ile, na wewe unasalimu amri kwa uwoga tu bila kuuliza sababu au kutaka kujua haki zako. Baada ya hapo unaanza mzunguko wa mabishano na usumbufu usiokuwa na maana kutokana na kutotambua haki, sheria na taratibu.
*Tambua, nimetoa mfano huu kuonyesha chanzo cha tukio, sio kufananisha matukio. Sababu kuu ni kujua haki, sheria na utaratibu.*
Msanii Lady Jay Dee aliamua kuitaarifu jamii kuhusu hisia zake na matakwa yake ya baadae. Alitoa lawama kwa kituo cha redio na wamiliki wake. Siku zilizofuata Ruge akajibu yaliyojiri kutokana na habari kuwa kubwa zaidi. Kuna mambo mawili ambayo ninayaona kutokana na tukio hili.
- Haya yanayotokea hayajaanza leo (miaka hii), yamekuwapo kwa miaka mingi sana lakini kwa kiwango tofauti. Ukiwauliza wasanii/wanamuziki wakongwe, watakueleza mambo waliyopitia - na watakueleza kuwa wakati huo yalikuwa mabaya zaidi ya hivi sasa. Wanaweza kuelezea vituko vya wakati huo kwa kuelimisha na sio kuleta uhasama maana wamepitia tayari hali hiyo na wanaijua - kwahiyo hawawezi kujenga hisia kuzunguka tukio.
- Hakuna ushindani kwenye suala hilo - kama ni mshindi, basi wote wameshinda; kama kushindwa, basi wote wameshindwa. Kwa nini? Pande zote mbili zimejitoa muhanga kurekebisha mazingira yasiyokuwa na uwiano. Ukiangalia kwa umbali zaidi, utaona ni ushindi kwa tasnia nzima - maana itakuwa somo kwa wengine.
Tukiachana na wahusika binafsi, chombo cha habari kimeguswa. Jamii imeguswa, maana ni wateja wa chombo cha habari. Wengine wanasema kuwa chombo cha habari kimekosea kuruhusu hisia binafsi kutangazwa kwenye jamii kwa namna ilivyofanyika. Kuna taratibu na sheria zinazoongoza vyombo vya habari, pia kuna mamlaka zinazisimamia sheria hizo.
Mapendekezo ya Wadau ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (2011). Sura ya Nne ya muswada huo inaelezea kuhusu Uwajibikaji Wa Vyombo Vya Habari. Kwenye Sura 4. 30 (2) 'Litakuwa jukumu la kila mhariri au mwendeshaji wa vipindi katika kila chombo cha habari kujiridhisha kuwa yaliyomo katika makala, maoni, habari, hoja au mchango uliofanywa na Umma katika chombo hicho haukiuki kanuni za maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.'
Kwa namna fulani, shirikisho au chama kwa ajili ya kusimamia na kulinda haki za wasanii na wanamuziki ni muhimu sana katika mazingira haya.
Kwahiyo, ni busara kulitazama suala hili kama nafasi ya kuweka kinga kwa pande zote mbili kuepuka marudio hapo baadae. Kumbukeni hili suala sio la kisiasa. Siasa isiruhusiwe kuchafua zaidi burudani ya jamii kwa manufaa ya wachache.
Nimekusoma na kukuelewa vyema Gota,mimi mtazamo wangu katika hili suala ni juu ya matumizi ya vyombo vya habari hasa ikizingatiwa kuwa tunazo sheria lakini mtu anapokiuka sheria hiyo na hakuna hatua zozote anazochukuliwa ni wazi kuwa zipo hisia za siasa katika jambo hili lisilohotaji hata harufu ya siasa......yapo mengi kuzungumzia hili lakini niseme tu kuwa tatizo haliwezi kumalizwa kwa tatizo na ndio maana nashangaa sana namna ambavyo wasanii wanavyogawanywa bila kujitambua kuwa wao ndio wenye ngu8vu......ni jukumu letu sote kuelimishana na kupambana na siasa hizi,mwisho ningependa kila mtu atafute wimbo wa marehemu Justine Kalikawe uitwao TATIZo ausikilize halafu tuendelee kuchukua hatua!
ReplyDelete