Siku chache baadae, tunasoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa waziri fulani amejitosa kwenye sakata hilo. Ataogelea kweli kweli!
Kwanza nianze na uandishi wa habari - lengo kuu ni kutafuta, kuchambua, kuchunguza, kuhariri na kutangaza habari kwa jamii. Sasa kuna habari ya 'kujitosa' ambayo mwandishi anaandika 'Lakini jana katika taarifa yake hapa,...'. Nia yangu ilikuwa kujua 'hapa' ni wapi?! Ni wapi taarifa hiyo ilipotolewa? Kwa kuwa ni habari inayoeleweka, niliamua kusoma habari yote nielewe nini kimeandikwa.
Nilivyosoma, nikaona Naibu Waziri ametoa 'mwito nikutane na pande mbili.' Hilo ni jambo zuri sana katika uwanja wa usuluhishi.
Nilipata maswali mengi sana kichwani kutaka kujua mwelekeo wa sakata hili. Lakini nikakumbuka onyo kuwa 'hili suala sio la kisiasa'. Sasa ni mtazamo wangu!
Burudani na siasa ni sawa sawa na wachumba wa muda mrefu ambao wanagombana na kuachana, baadae kurudiana tena; na kila wakati wanatongozana tu. Mfano Fela Kuti, kwenye muziki wake alikuwa anagusia mambo ya siasa. Uhusiano wake na wanasiasa unajulikana dunia nzima. Burudani kwa ujumla lazima itaingilia siasa kwa namna fulani. Unaweza ukatungwa wimbo wa uchochezi katika jamii; utapigwa marufuku na kujadiliwa. Kwahiyo, mambo yanayofichua lazima yapate pingamizi.
Kutokana na ukweli kwamba zipo mamlaka ambazo zinasimamia utungaji wa sera, sheria na taratibu. Upande wa burudani unakuwa na mapambano na mazingira ya hizo sera, sheria na taratibu ambayo yamewekwa na mamlaka hizo. Mambo kama hayo ndio yanaleta muingiliano kati ya burudani na siasa. Na sio ushindani - kila upande unakuwa na ushindi wake katika muda na nafasi fulani. Huo ndio uhusiano wa siasa na burudani.
Kwenye sakata hili, maswali ni mengi sana yanayohitaji majibu - na sasa waziri ambaye ni mwakilishi wa serikali 'anajitosa' kusuluhisha.
- Kwani hili sakata linahusiana vipi na serikali?
- Au wahusika wanahusiana vipi na serikali hadi kuitwa kusuluhishwa na waziri?
- Ni waziri na wahusika, au wahusika na serikali?
- Tatizo ni binafsi au la kitaifa?
- Kama ni mgongano binafsi; wahusika wanalipa kodi kiasi gani hadi kusuluhishwa na kodi za wananchi? (Mwananchi anataka kujua.)
Waziri 'Msuluhishi', wewe ni mwakilishi wa serikali. Kuna mambo ambayo inabidi ufahamu:-
Hili sakata ni kati ya watu binafsi, inakuwaje wewe kiongozi wa kitaifa unaingilia mzozo wa watu binafsi? Ni aibu kwa jamii 'kujitosa' kwenye malumbano ya watu binafsi. Waache, watamalizana wenyewe, wanajuana.
Kwa nafasi yako nadhani ungekubali kuwa malumbano hayo hayana tija kwa jamii na kutumia uwezo wako na wizara yako na wengine wote wanaohusika kurekebisha uozo huo ambao upo kwenye biashara ya muziki.
Wapo wengi ambao wapo katika mazingira kama ya mlalamikaji, tena ni wengi na katika hali mbaya zaidi ya huyo aliyelalamika. Unajua hiyo?
Mimi sioni kama hilo sakata ni la kitaifa hadi waziri 'kujitosa'. Mimi ninaona ni mbwembwe za biashara ya muziki. Kama ni la kitaifa, tufafanulie.
Kundelea kuendekeza tabia za kijinga ambazo jamii isingependa kuona inatokea, ni kurudisha nyuma maendeleo. Biashara ya muziki imeoza kutokana na mamlaka husika kushindwa kusimamia sera na sheria ambazo zimewekwa. Jamii imekuwa 'inalishwa' upuuzi hadi leo hii watoto wetu wanatembea matako nje; wengine wanaona ngono ndio burudani ya mwisho duniani; wasichana wanaonyesha maungo yao bila aibu. Mbona mambo hayo hayazungumziwi kama ni maadili yasiyokwenda sawa tabia ya Mtanzania?
Pia wapo wadau wengine ambao wameguswa na haya yanayoendelea. Kama wanahabari na wasanii. Tafadhali acheni unafiki na ushabiki. Wasanii tambueni nafasi yenu kwenye biashara ya muziki. Waandishi mmekuwa washabiki zaidi ya kuhabarisha na kuelimisha jamii. Biashara ya muziki/burudani ipo huru ndani ya mipaka yake, najua itaendelea kuwa hivyo.
Hakuna hisia hapo, ni mtazamo wa Gotta!!!!
No comments:
Post a Comment